Vifaru vyengine kumi vya Uturuki Alhamisi (25.08.2016) vimevuka mpaka 
kuingia Syria siku moja baada ya wapiganaji wa upinzani wa Syria 
wanaoungwa mkono na Uturuki kuwatimuwa wanajihadi katika mji wa 
Jarabulus.
Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema hapo jana kwamba mashambulio yao yamelitimuwa kundi la Dola la Kiislamu kutoka kwenye mji wa Jarabulus na waasi wanaoungwa mkono na serikali ya Uturuki wameripoti kwamba wapiganaji hao wa jihadi wamerudi nyuma kuelekea kusini mwa mji wa Al- Bab.
Mlolongo mpya wa vifaru ulikuwa ukirindima kwenye barabara chafu maghaibi mwa mji wa mpakani wa Uturuki wa Karkamis na kutimua vumbi hewani kabla ya kuvuka mpaka.Vifaru hivyo baadae vilifuatiwa na magari ya deraya.
                                                    Operesheni kubwa kabisa
Operesheni hiyo kubwa kabisa kuwahi kuanzishwa na Uturuki katika kipindi
 cha miaka mitano na nusu ya mzozo wa Syria imeviweka nchi kavu vikosi 
maalum vya Uturuki na ndege zake za kivita zikishambulia maeneo ya kundi
 la Dola la Kiislamu. 
Ndege hizo zinasaidia mashambulizi ya ardhini yanayofanywa na mamia ya waasi wa Syria ambao hapo jana waliingia katika mji wa Jarabulus na vijiji vya jirani bila ya kukabiliwa na upinzani mkubwa.
| Mashambulizi ya Uturuki nchini Syria. | 
Waziri Mkuu wa Uturuki Binali Yildrim amekiambia kituo cha televisheni 
cha Haberturk katika mahojiano kwamba wapiganaji wa upinzani wa Syria 
wamebakia katika mji wa Jarabulus na wameanza kudhibiti miji na vijiji.
                                       Wakurdi wawe sehemu ya ufumbuzi
Hapo jana mwanasiasa mwandamizi wa Kikurdi nchini Iraq ambaye ni mjumbe 
wa baraza la uongozi Ali Hussein amesema vyama vya kisiasa nchini Syria 
havina budi kuchukuwa hatua ambazo hazitokuwa tishio kwa usalama wa 
kanda hiyo baada ya Uturuki kutuma vifaru vyake nchini humo. 
Hussein amesema "Tumewashauri na kuwashajiisha Wakurdi walioko nchini 
Syria wasikubali kukiachilia hata chama kimoja au kundi moja kuhodhi na 
kutumia kwa hila mamlaka ya kujiamulia mambo yao. Wakurdi na Wasyria 
wengine wote wanaweza kushirikiana kwa faida yao ya pamoja.Inabidi 
wajaribu kufikia makubaliano ya kisiasa.Hawapaswi kuwa sehemu ya tatizo 
nchini Syria bali wawe sehemu ya ufumbuzi nchini humo."
| Mpiganaji wa Kikurdi nchini Syria. | 
Serikali ya Uturuki imesema hapo jana kwamba itaendeleza operesheni zake hadi hapo itakapokuwa imeamini kwamba vitisho dhidi ya usalama wake wa taifa vimedhibitiwa.

No comments:
Post a Comment