Most Popular

Kuapishwa rais mpya nchini Brazil katika anga ya mgogoro wa kisiasa na kiuchumi

Michel Temer, rais wa muda nchini Brazil amekula kiapo kama rais mpya wa nchi hiyo.

Mbali na Temer kuahidi kufanya juhudi kwa ajili ya kuokoa uchumi wa Brazil kutokana na mdororo, amesisitiza pia kwamba, hivi sasa na baada ya kuenguliwa madarakani Rais Dilma Rousseff, umefika wakati wa kuiunganisha nchi hiyo. Katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa na baada ya kuapishwa,

Rais wa zamani wa Brazil Bi Rousseff akiwa na rais wa sasa wa nchi hiyo
Michel Temer amesema kuwa, hivi sasa Brazil inahitaji uthabiti wa kisiasa kwa ajili ya wawekezaji wa kigeni. Rais mpya wa Brazil ameapishwa katika hali ambayo wapinzani wake wamemiminika mabarabarani.

 Maandamano ya wapinzani hao wanaomuunga mkono Dilma Rousseff, yamekabiliwa na polisi wa nchi hiyo. Wakati huo huo wakili wa rais aliyeondolewa madarakani ameitaka mahakama kuu ya nchi hiyo kuchunguza upya faili la mteja wake. Inafaa kufahamika kuwa, siku chache zilizopita, wawakilishi wa bunge wapatao 61 walimuuzulu

Rais Rousseff kutokana na kile walichosema kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za serikali. Rousseff alikuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Brazil ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2014 alichaguliwa kwa muhula wa pili ndani ya taifa hilo. Hata hivyo kufeli sera zake za kiuchumi na matukio yaliyojiri hivi karibuni kuhusiana na tuhuma kadhaa za ufisadi zilizolikumba Shirika la Mafuta la Serikali la Petrobras, kulipelekea kuibuka mgogoro wa kisiasa nchini humo. Shirika hilo linatuhumiwa kwa kudhamini kiasi kikubwa cha fedha kwenye kampeni za uchaguzi wa mwaka 2014 kwa ajili ya Rais Dilma Rousseff. Kwa mujibu wa wapinzani wa rais huyo aliyeuzuliwa madarakani, shirika hilo pia lilihusika katika kudhamini fedha za kampeni za Rousseff katika uchaguzi wa mwaka 2010

Hii ni katika hali ambayo Bi, Rousseff mwenyewe amekana kuhusika kwa aina yoyote ile na ufisadi huo. Ukweli ni kwamba mjadala wa kisiasa nchini Brazil bado unaendelea. Vutanikuvute hizo za kisiasa zilizoshuhudiwa miezi michache iliyopita dhidi ya Rais Rousseff zilizofanywa na wapinzani wake, zilisababisha kupooza serikali ya Brasília na hata katika mashindano ya Olimpiki yaliyomalizika hivi karibuni nchini humo, wangwi wa msuguano huo uliendelea kusikika.

 Aidha matukio hayo yametia doa jihudi za serikali ya Brazil kwa ajili ya kukabiliana na mporomoko wa uchumi wa taifa hilo lenye uchumi mkubwa katika eneo la Amerika ya Kusini. Kuporomoka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, ni jambo lingine lililopigilia msumari wa matatizo ya kiuchumi nchini Brazil, na hivyo kuongezeka umasikini na ukosefu wa ajira. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, Michel Temer Rais wa sasa wa Brazil ambaye pia ni mkuu wa chama cha Kidemokrasia nchini humo, alikuwa mshirika wa serikali ya muungano iliyokuwa ikiongozwa na Rousseff na kwa kipindi cha miaka 13 iliyopita alikuwa ndani ya serikali huku akiwa na faili sawa na la rais aliyeuzuliwa madarakani.

Viongozi wa mrengo wa kushoto nchini humo kama ilivyo kwa nchi nyingine za Amerika ya Kusini, wanafahamu kwamba kiini cha migogoro ya eneo hilo kinatokana na uingiliaji wa kigeni. Kwa mujibu wa viongozi hao, matukio yote yanasababishwa na siasa chafu za Marekani katika eneo. Hii ni kusema kuwa, kwa kipindi chote cha historia, Marekani imekuwa ikiichukulia Amerika ya Kusini kama chumo la tonge lake na ni kwa msingi huo ndio maana eneo hilo likapewa umuhimu maalumu na viongozi wa Washington.

Kwa mujibu wa viongozi hao wa mrengo wa kushoto nchini Brazil, uchochezi wa Marekani katika kuuzuliwa madarakani Rais Dilma Rousseff, si jambo jingine ila ni kukabiliana na matakwa ya wananchi wanaotaka uhuru na kujitegemea.

Weledi wengi wanaamini kwamba, kuuzuliwa Rousseff na kuwekwa mahala pake Michel Temer, hakuwezi kumaliza matatizo ya kisasa ya kisiasa na kiuchumi katika jamii ya Wabrazil. Inaonekana kwamba kuitishwa uchaguzi wa mapema wa rais na bunge, ndiyo ingekuwa njia bora ya kuhitimisha mgogoro wa kisiasa nchini, hata hivyo hatua ya kuingia madarakani Michel Temer, ni jambo ambalo halidhaniwi kama litakalosaidia kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa taifa hilo.


Posted By: MJOMBA ZECODER

Kuapishwa rais mpya nchini Brazil katika anga ya mgogoro wa kisiasa na kiuchumi

No comments:

Post a Comment

About Us

Advertisment

Like Us

© WWH-WORLD WIDE HABARI All rights reserved | Theme Designed by Mjomba Computers Published.. Blogger