Shirika la habari la serikali ya
Korea Kaskazini limesema taifa hilo limefanya majaribio ya bomu kupima
uwezo wa bomu lake la nyuklia la kurushwa kwa kombora hatua ambayo
imeshutumiwa vikali na jamii ya kimataifa.
Tetemeko hilo lilikuwa na nguvu ya 5.3 kwenye vipimo vya Richter.
Maafisa wa jeshi la Korea Kusini wanakadiria kwamba mlipuko huo ulikuwa sawa na wa kilo tani kumi za TNT, ukubwa sawa na wa bomu lililoangushwa Hiroshima na Marekani wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia. Baadhi wanasema huenda bomu hilo la Korea Kaskazini likawa lilikuwa na nguvu ya kilo tani 20.
![]() |
Rais Kim Jong-un ameonyeshwa kwenye runinga akiwa amejaa tabasamu |
Bomu lenye nguvu zaidi la nyuklia lililowahi kulipuliwa lilikuwa lile lililopewa jina Tsar-bomba, ambalo lililipuliwa na Urusi mwaka 1961.
Lilikuwa na nguvu ya mega tani 50, sawa na nguvu ya tani milioni 50 za TNT (50,000,000).
Wataalamu bado wanaendelea kudadisi iwapo lilikuwa bomu la haidrojeni, jambo ambalo linaweza kulipa nguvu zaidi kushinda mlipuko wa bomu la kawaida la nyuklia.
Hilo likithibitishwa, basi itakuwa ni mara ya tano kwa Pyongyang kutekeleza jaribio la silaha za kinyuklia.
Jaribio la leo limetekelezwa siku ambayo serikali inaadhimisha kuanzishwa kwa taifa la sasa la Korea Kaskazini mwaka 1948.
Jamii ya kimataifa imeghadhabishwa na hatua hiyo ya Korea Kaskazini.
Rais wa Korea Kusini Park Geun-hye ametaja jaribio hilo kuwa "jaribio la kujiangamiza" ambalo linaonyesha "kutomakinika" kwa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un.
Bi Park, ambaye amesitisha ghafla ziara yake ng'ambo, amesema baada ya kutekeleza jaribio hilo la tano la nyuklia "serikali ya Kim Jong-un itakaribisha vikwazo zaidi na kutengwa zaidi na jamii ya kimataifa."
Bi Park alifanya pia amzungumzo ya dharura na Rais wa Marekani Barack Obama kwa njia ya simu.
Kuvumiliwa
China, mshirika mkuu wa Korea Kaskazini kidiplomasia, pia imeshutumu hatua hiyo na kuihimiza Pyongyang kukoma kuchukua hatua ambazo zinaweza kuzidisha hali.Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe, amesema majaribio kama hayo ya Korea Kaskazini hayawezi kuvumiliwa.
Lakini mwandishi wa shirika la habari la BBC anayeangazia Korea anasema wapinzani wa Pyongyang wanatatizika kuhusu ni hatua gani wanafaa kuuchukulia utawala wa Korea Kaskazini.
Tayari waliwekea taifa hilo vikwazo Januari baada ya Pyongyang kufanya jaribio la nne ya nyuklia.
No comments:
Post a Comment