Wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, wakiwa kwenye moja ya mikutano ya chama hicho wakati wa kampeni za urais mwaka jana. |
Uamuzi wa msajili wa vyama kuingilia kati mvutano huu, imekuja baada ya chama kikuu cha upinzani nchini humo, CHADEMA, kusisitiza azma yake ya kufanya maandamano ya nchi nzima September mosi mwaka huu kupinga hatua ya Serikali kukataza kufanya mikutano ya kisiasa.
Mbali na CHADEMA ambao wamepanga kufanya maandamano waliyoyaita UKUTA, chama tawala CCM kupitia umoja wa vijana wa chama hicho UVCCM, nao walikuwa wameomba kibali cha kufanya maandamano tarehe 30 ya mwezi huu.
Kwa miezi kadhaa sasa jeshi la Polisi nchini Tanzania limepiga marufuku kufanyika kwa mikutano yoyote ya kisiasa kwa kile jeshi hilo linasema ni kwasababu za kiusalama, hatua ambayo upinzani unasema ni kuminya uhuru wa vyama vya siasa kufanya mikutano ya ujenzi wa vyama vyao kwa uhuru.
Uamuzi wa jeshi la Polisi, ulitokana na kauli aliyoitoa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, ambaye aliagiza jeshi hilo kuzuia mikutano yoyote ya kisiasa, kwa kile alichosema kuwa huu sio wakati wa kufanya siasa na badala yake wanaotaka kufanya mikutano waifanye kwenye majimbo yao waliyochaguliwa.
![]() |
Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania, jaji mstaafu Francis Mutungi |
Akizungumza jijini Dar es Salaam, juma hili, jaji Mutungi amesema si jambo la busara kwa vyama vya siasa kukaidi miongozo na sheria zilizopo, na badala yake njia nzuri ya kutatua sintofahamu iliyopo ni kwa viongozi hao kukutana.
Jaji Mutungi amevitaka vyama vya siasa vilivyopanga kufanya maandamano mwishoni mwa mwezi na mwanzoni mwa mwezi ujao, kuahirisha maandamano hayo na badala yake waitikie wito wake wa kukaa kwenye meza ya mazungumzo.
Baada ya kauli hiyo, CHADEMA imetoa taarifa kuunga mkono wito wa jaji Mutungi, lakini kikaonya kuwa kitashiriki kwenye mazungumzo hayo ikiwa yanania ya dhati kutetea na kuilinda katiba ya nchi kuhusu uhuru wa vyama vya siasa kutekeleza majukumu yao bila kuingiliwa.
No comments:
Post a Comment